Wednesday, February 20, 2008

Jeshi La Polisi Lacheza Kizungu Mkuti.

Ikiwa ni masaa kadhaa tangu wana Jamboforums kuachiwa kwa dhamana na jeshi la polisi. Ni kweli ya kwamba jeshi hilo liliwashikilia Watanzania hawa kwa misingi ya kibabe, misingi ya kijesusi ambayo imetumika zama zile za ulanguzi na ubepari. Akihojiwa na BBC swahili (www.bbc.co.uk/swahili) mzungumzaji mkuu wa jeshi hilo alionekana kujitafuna tafuna pasipo kueleza ni nini makosa ya wana Jamboforums hao.

Habari tulizonazo kutoka klh news (www.klhnews.com) zinathibitishwa kuachiwa kwa wana jamboforums hao. Vile vile wana jamboforum wengi duniani wamenukululiwa kukikemea kitendo hicho cha kikoloni cha kukamata watu pasipo hatia. Hata hivyo jeshi la polisi limeendelea kutupakazia wana jamboforum mambo yasio na kichwa wala miguu, mambo kama Jamboforum ni website ya ngono, ni website ya kigaidi na mengine mengi.

Wito wa wana Jamboforum kwenda kwa wanaserikali ni kwamba, Jamboforum haina mahusiano yoyote na chama chochote cha kisiasa nchini Tanzania, Jamboforum haitokufa wala haitodhibiti haki ya wanchi kuzungumza, jamboforum haitoacha kukemea, kukosoa na kushutumu vitendo vyovyote vile vya kinyonyaji vitakavyofanywa na serikali ya awamu yoyote au ya chama chochote nchini Tanzania. Vile vile jamboforum itaendeleza wimbi lake lile lile la kusifia maamuzi mazuri ya serikali pindi yafanyikapo, na vile vile kukosoa maamuzi ya kihayawani kama Richmond, IPTL, Dowas, na Mengine mengi.

Kila mwanadamu ana haki ya kuzungumza iwe ni kwa ana kwa ana, au iwe kwa kutumia nick name kwenye internet au iwe kwa kutumia jina lake kwenye gazeti, si haki ya serikali huru yoyote kuzuia uhuru wa kusungumza. Imefika muda kukemea mambo haya ya kijasusi ambayo jeshi la polisi la Tanzania linayafanya. Kukamata vijana hawa kuna tofauti gani na kumwagia waandishi tindikali? karne ya ishirini na mmoja inahitaji serikali yenye ufanisi wa mambo yake, na sio serikali yenye miundo mbinu ya kijasusi.

Mungu ibariki Africa, Mungu ibariki Tanzania.
Asanteni

No comments: